Ukiwa mtu wa
kuangalia mambo kwa juu juu basi kila kitu kwako kitakuwa kigumu. Kusoma
unaweza kuona ni kugumu, kufanya kazi kugumu, hata kusubiri mshahara unaweza kuona
ni kugumu.
Urahisi kwako unaweza kuwa katika kutumia
pesa, pengine na kula tu. Ila watu
waelevu na wenye uvumilivu kwako kila kitu kinaweza kuwa tofauti na wewe.
Unachoona kigumu kwao wanahisi si ugumu bali
ni changamoto za kuzidisha jitihada na umakini tu. Kwenye mapenzi pia hali
haiko tofauti sana. Wale wanao achana kila siku si kama ndiyo wanakosewa sana
kuliko wale ambao hawaachani, hapana. Suala ni lile lile tu.
Wakati wengine wakiona tofauti zao ni kama
changamoto za kusomana tabia na kuamua kuishi kutokana na kila mmoja kumjua
mwenzake. Wenzao wanaona suluhisho la yote ni kila mmoja kuwa na maisha yake.
Suala la uvumilivu kwao hamna.
Hakuna mapenzi duniani yanayoweza kushamiri
bila suala hili. Usipokuwa na moyo wa uvumilivu katika mapenzi basi kila mtu
utamuona hafai. Utamuona hafai na kila siku utakuwa mtu wa kuanzisha mahusiano
mapya. Hayo si maisha sasa!
Mahusiano yaliyodumu si kwa kuwa wahusika
hawakoseani au makosa wanayokoseana ni madogo sana. Hapana. Kila binaadamu ana mapungufu
yake. Wote huwa wanakoseana ila tofauti yake na wengine ni kwamba busara na
uvumilivu huwa msingi wa mapenzi yao na ndiyo maana tunaona wanadumu mpaka leo.
Ni binaadamu gani unaweza kuishi naye na msikosane?
Ni nani mwenye uwezo wa kukupa unachotaka kila siku? Hakuna binaadamu wa aina
hiyo.
Hivyo unavyotaka kuachana na uliye naye
suala la kujiuliza ni kuwa mara ngapi umemueleza kuhusiana na suala unalotaka
kumuachia. Na hiyo isitoshte tu pia jiulize ni sababu gani inayomfanya kutenda
suala hilo. Ukimaliza hapo rudi nyuma na jiulize tena huwa unatumia maneno ya
aina gani katika kumkanya.
Maana wengine baada ya kukosewa wao huwa
hawawakanyi vyema wenzao wao bali huripuka kwa maneno makali na dharau. Matokeo
yake sasa wahusika badala ya kuwasikiliza na kufanyia kazi maneno wanayoambiwa
kutokana na makosa yao. wao huwapuuzia na kwaona ni wasema hovyo.
Ndiyo, kukosewa kunaumiza sana ila jiulize
ni kitu gani kimetokea bila sababu? Kwenye makosa ya mpenzi wako kuna sababu
nyuma yake, hebu itafute badala ya kulalamika.
Mapenzi yasiyo kuwa na uvumilivu ndani yake
hayana maisha marefu. Kwa sababu binaadamu ni kiumbe mwenye kukosea.
Badala
ya kukimbilia kuachana ebu geuka kuwa mwalimu wa mpenzi wako angalau kwa mara
chache.
Mpenzi wako ni furaha yako kwa maana ndiyo
mtu uliyeridhia naye kuwa naye katika masuala nyeti yahusuyo maisha yako. Sasa
kwanini uwe tayari kumpoteza kisa kachelewa kurudi. Kuwa mvumilivu . Watu wenye
hekima ni wavumilivu. Watu wenye kujielewa ni wavumilivu.
Ukiwa hauna uvumuilivu kila siku utatangaza
ndoa. Leo utaachana na Mugambara kwa sababu anaongea sana na wasichana ila, jua
huyo unaeenda kuwa naye anapenda sana kitu ambacho hukipendi. Anakunywa pombe
je, utawezana naye? Jibu unalo.
Kwa
kuwa huyo uliye naye unampenda kwa dhati basi amua kwenda naye taratibu
ukijitahidi kumbadilisha tabia zake. Usiogope, inawezekana, suala ni uvumilivu
na kujiamini tu. Kukubali kumpoteza unayempenda kwa kukosa uvumilivu ni
kujitakia kuingia katika maisha ya kutanga tanga tu.
Kumbuka, siku zote wanaovumilia ndiyo huwa
wanabaki na ushindi.Bila uvumilivu Mandela asingekuja kuwa raisi wa afrika
kusini.Uvumilivu ni kila kitu katika maisha.
ramadhanimasenga@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni