Mapenzi ni
kitu cha tofauti kidogo. Umeshawahi kuona watu wakiwa ndani ya mapenzi moto
moto? Umeshaona wanavyokuwa wakiwa pamoja? Hata kama wana miaka sitini ila
wakati mwingine huwezi kutofautisha matendo yako na watoto.
Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi yake
ili uweze kuyaelewa vizuri.
Mapenzi yanalugha ya ajabu sana. wakati unapoweza
kumjibu rafiki yako “poa tu” na isilete matatizo ila katika mapenzi hapa kuna
tatizo. Hapo mwenzako anaweza kuhisi umekasirika, anaweza kudhani sasa hivi
humuheshimu kama zamani – ilmradi tu. Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi
zaidi.
Kila unachofanya kwa mpenzi wako kina maana kubwa hata kama hujadhamiria.
Unapopokea simu haraka anapokupigia inaleta maana f’lani kwake hata
unapochelewa pia anapata maana. Tofauti ni moja tu, pale atapata maana nzuri
kuwa unamjali na kumuheshimu wakati huku atapata maana hasi- inayoweza kumpa wasi wasi na wahka katika
nafsi yake. Katika mapenzi hakuna kitu kidogo!
Simu yako kwake ina maana, sms yako ina
maana hata aina ya utani unaomletea pia unamletea tafsiri f’lani katika akili
yake. Kuna utani mwingine ukimfanyia anajiuliza mmmh… ni utani huu? Au
kafikisha ujumbe kwa namna tofauti? Hayo ndiyo mapenzi. Ambayo yanamfanya
mpenzi wako akuombe salio na ukimtumia yote anatumia kuongea na wewe, tena
ukiangalia kwa haraka unaweza kusema hakuna neno la maana alilokwambia.
Ila jua kitendo cha kukupigia simu tu kwake
na kwako pia kina maana. Kwake kukupigia simu ni faraja kubwa kwa sababu
kaongea na mtu anayemuamini na kumkabidhi hisia zake. Mtu ambaye ana mamlaka ya
kumuuliza jana kwanini ulichelewa kulala ama kwanini leo umevaa hivi. Mtu wa
kipekee aliyeamua kumruhusu kuwa na neno juu ya maisha yake. Hayo ndiyo
mapenzi!
Anakupigia mara kwa mara si kwa sababu hana
watu wengine wa kuongea nao - hapana. Ni
kwa kuwa anakujali na kukuthamini. Ukiona suala hilo ni dogo basi mwenzako ataona
humthamini wala kumjali. Ataona unamdharu. Ataona anajipendekeza kwako.
Unajua matokeo ya fikra za namna hiyo
zikimea katika kichwa chake? Ni kujiona hayuko na mtu sahihi katika maisha.
Thamini kila unachofanyiwa na mwenzako bila
kuangalia ukubwa wala thamani yake. Katika mapenzi kila jambo lina nafasi yake
ya kuyajenga ama kuyabomoa mahusiano yenu. Ukiona kumpigia sana simu ni usumbufu,
we acha tu. Ukiona kumwita majina ya kimapenzi mwenzako si kitu, sawa tu. Ila unapaswa
kukaa tayari kwa matokeo ya bomu unalotengeneza. Ukae vizuri pale mwenzako
atakapokwambia ama kuwaeleza marafiki zake humjali wala humthamini.
Vijengavyo mapenzi ya kweli si magari na
kupelekana ‘out’ Dubai tu ila ni kila jambo la kimapenzi ulifanyalo kwa mwenzi
wako bila kujali ukubwa wala thamani yake.
Thamani ya tendo unalomfanyia mwenzako
litaamuliwa na kiwango cha hisia alicho nacho juu yako nafsini kwake. Kama mtu
hana hisia na wewe hata umfanyie nini atafurahi na kukuona wa kawaida tu ama
mwenye pesa sana. suala ni hisia. Mapenzi ni hisia.
Na
mwenye hisia na wewe kila jambo kwake ni muhimu. kauli ndogo tu zimeweza
kurejesha amani na upendo katika nyumba nyingi, pia kauli zingine ambazo pia ni
ndogo zimesababisha nyumba nyingi kuvunjika. Kuwa makini na matendo na kauli
zako kwa mwenzako. Hakuna kidogo katika mapenzi. Kila jambo lina thamani yake.
ramadhanimasenga@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni