Uhusiano wa
mapenzi ni muunganiko wa hiyari wa watu wawili wenye kupendana,kukubaliana na
walio tayari kuvumiliana na kurekebishana pale inapobidi. Hiyo ni moja kati ya
tafsiri rahisi ya uhusiano wa mapenzi.
Mtu yoyote aliyekuwapo katika mahusiano
anatakiwa kuwa tayari kumsikiliza mwenzake, kumvumilia na kubadilika kitabia
pale inapopaswa kuwa hivyo.
Na kwa kuwa suala la mapenzi ni suala ambalo
huwakutanisha watu ambao hupendana basi mambo mengi hukuta yakienda ‘Automatically’
au bila kutumia nguvu kubwa katika kuyabadilisha. Hata kama mmoja alikuwa mlevi
sana au tabia nyingine yenye kukera,basi huweza kubadilika kwa lengo la
kumfanya mwenzake awe na furaha.
Kama kweli ana upendo na wewe, kubadilika
ni suala ambalo atalipa kipaumbele hata kama litachukua muda mrefu kiasi gani. Watu
wenye kupendana kwa dhati hupenda kusikilizana na kuridhiana katika yale mambo
ambayo huona inafaa kufanya hivyo.
Si jambo la kawaida hata kidogo kukuta
malumbano ya kila siku katika nyumba ya watu wanaopendana kwa dhati. Upendo
huwafanya waishi kwa amani na masikilizano.
Nguvu ya upendo huwafanya hata wenye historia tofauti katika maisha
kusionekane tofauti baina yao. Huwafanya wasomi na wasiokuwa wasomi wajione ni sawa.
Lakini hali huwa tofauti katika nyumba isiyokuwa na upendo.
Amani huwa shida. Ugomvi huwa karibu kila
siku. Hata vile vitu vidogo ambavyo huweza kumalizwa kwa busara hushindikana
mpaka kelele na maneno kadhaa ya kashfa yachukue nafasi. Kila mmoja hujiona yuko
juu ya mwenzie.
Msomi atataka kuonesha usomi wake hata pale
asipoweza kufanya hivyo. Mrembo atataka kudhihirisha hilo mbele ya mpenzi wake,
ilimradi tu.Kisa?
Upendo baina yao hakuna. Laiti kama ungekuwapo pasingekuwapo madaraja
baina yao. Hakuna ambaye angejiona yuko juu ya mwenzake. Wote wangejiona sawa.
Katika majumba mengi kuna kesi nyingi baina
ya wanandoa. Kila siku kama si kuitwa mshenga basi ni safari kwenda kuomba
nasaha kwa wazazi. Ndoa nyingi zinaishi kwa ajili ya busara ya wazazi na si
upendo uliopo baina ya wahusika.
Wanawake wengi wanatoa uroda kwa waume zao
kutimiza wajibu tu. Wanaume wengi katika majumba yao wanawahi kurudi nyumbani
kwa sababu ya kuogopa kuitwa katika vikao na wazazi. Ukichunguza chanzo cha
yote utapata jibu hili.
Upendo baina yao hakuna au umeanza kufifia.
Ukiishi na mtu unayempenda si mara kwa mara kesi zenu zitahitaji hakimu kutoka
nje. Mara nyingi mambo yenu mtaweza kuyamaliza ndani hata majirani wasijue.
Kuishi
na mtu ambaye aidha ulichaguliwa au ulilazimika kumuoa kufuata kitu tofauti na
hisia za upendo juu yake ni janga.
Ni lazima utakutana na tabia za ajabu na asitake
kuzibadilisha. Kama alikuwa mlevi basi atakwambia alianza kulewa kabla hamjawa
pamoja, hivyo usimuingilie katika maisha yake. Kama ulimkuta ni mtu wa disco si
ajabu sana akikwambia muziki uko katika damu yake, kwa hiyo kama unataka
kuendelea kuishi naye basi itabidi ukubaliane na kila unachomuona nacho.
Kumjua
mtu akupendaye kwa dhati wala ahihitaji shahada ya chuo kikuu. Yatazame matendo
yake, angalie jinsi anavyoonesha kukujali, mwangalie jinsi atakavyokuwa anajali
furaha yako. Kisha changanua kama matendo yake kwako yanakupa furaha na
yanahakikisha unapata amani katika nafsi yako.
Kutokana na wengi kulala usingizi wa
mapenzi, kuna kitu huwa tunashindwa kufahamu na kujikuta kila siku tunaumia
kichwa.
Watu wengi tunaumia kichwa kuwaambia wapenzi
wetu vitu tupendavyo ilhali wakiwa wanajua. Ila pia mbali na kutumia muda
mwingi katika kuwaambia vitu hivyo lakini mara nyingi huwa hawavifanyi na
matokeo yake kutuacha na majonzi na masikitiko makubwa. Narudia tena.
mtu akupendaye atapenda akuone na furaha na
amani. Hata siku moja hatopenda kukuona ukiumizwa na matendo yake. Acha kuumiza
sana kichwa na badala yake ishi na ukweli huu.
Kama kweli anakupenda kwa dhati angebadilika.
Acha kuchosha misuli ya kichwa kila siku kwa kusema neno moja.
ramadhanimasenga@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni