Uamuzi
unaochukua leo ndiyo wenye kuweza kukusababishia furaha au majuto baadaye.
Mambo mengi yaliotokea leo ni matokeo ya kile ulichokiamua jana. Iko hivyo na Hata katika mapenzi hali ni hiyo hiyo.
Uzuri
wa mahusiano yako ya leo umeamuliwa na uamuzi mzuri wa kusikiliza hisia zako na
kuamua kuwa na huyo uliye naye leo.
Huyo anayekufanya kila dakika uone thamani
na amani ya kuwa katika nyumba yako. Aliyefanya mahusiano yako yawe tofauti na
wale ambao Bar ni sehemu salama zaidi kwao kuliko katika nyumba zao. Ila hata
wao hali waliyo nayo leo ni matokeo ya kile walichoamua jana.
Uamuzi wako wa leo ni mbegu ya kitakachoota
kesho. Ukiamua leo kuwa na mtu usiyemuamini ni mbegu ambayo itazaa mahusiano ya wasi wasi.
Uliyenaye humtaki, na unaona suluhisho pekee ni kumuacha?
Sijui mnavyoishi hivyo siwezi kuliongelea
sana ila je, unaamini anastahili kuachwa? Sababu unazotaka ziwe kama sababu kuu
za kuachana kwenu zinaingia akilini? Mbali
na hilo amekosa sifa thabiti ya kuwa na wewe? Sifa ya kukupenda kwa dhati?
Kuachana kwenu leo kunatoa fursa ya yeye
kuwa huru mbali na wewe. Uhuru utakaompa nafasi ya kuangalia mwingine bila ya
nafsi yake kusutwa wala kuona hatia. Una uhakika unastahili kumuacha?
Una uhakika
kumuacha kwako si kupanda mbegu ya majuto itakayokutesa kesho? Mapungufu ni
suala la kila binaadamu, kama hiyo ndiyo sababu ya kutaka kumuachia futa. Kama
makosa anayofanya mpenzi wako japo yanaumiza ila anaonekana kuwa na nia madhubuti
ya kuyaacha pia hastahili kuachwa. Kuacha linaweza kuonekana kama tendo rahisi,
ila haliko hivyo.
Unamuacha leo huyo uliyemzoea ambaye unajua mapungufu yake ila mbali na yote una mapenzi
naye. Unayeenda kukutana naye unamjua? Haitoshi kusema unamjua eti kisa
umekutana naye mara mbili mara tatu. Si rahisi kumjua mtu vizuri kwa namna
hiyo. Tabia ya mtu utajua vizuri kwa kuongea naye mara kwa mara au kwa
kuishi naye. Hapo hawezi kuigiza tena.
Unapotaka kuachana na mtu ni vyema kwanza utulie kwa muda ukitafakari sababu za wewe kuachana naye na
hali ilivyo. Si vyema kuachana naye wakati una hasira. Ukifanya hivyo ni wazi
hautotoa uamuzi sahihi, uamuzi utakaoutoa hapo si ajabu baadaye kuujutia sana.
Hata siku moja hasira haifai kuwa kiongozi
katika kufikia maamuzi. Wengi bila kujua hili walijikuta walipogombana na
wapenzi wao bila kutafakari wakajikuta wakitaka kuachana, na matokeo yake sasa
wakiwaona wapenzi wao wapo na watu wengine mioyo inawauma. Kila wanapowaona
wapenzi wao wanahisi hawajawatendea haki kuwa na watu wengine, bila kujua kuwa
uamuzi wake ndiyo sababu ya yote.
Ni
kweli, wakati mwingine mtu unajikuta unafanya vitu bila kutarajia,ila unapoona
umekosewa na mpenzi wako hebu kaa naye mbali kwa muda, ili ujipe muda wa
kutafakari. Katika muda huo unaojipa ndiyo utaweza kupima ukubwa wa kosa la
mpenzi wako na adhabu stahili unayopaswa kumpatia.
Uamuzi wa kuachana haupaswi kuwa kimbilio ukifanyiwa
makosa. Ni rahisi sana kuona unafanya uamuzi sahihi leo kwa kufanya hivyo ila
jua unapoteza vitu vingi ambavyo havipatikani kwa urahisi.
Unampoteza mtu unayempenda kwanza, pia
unampoteza mtu ambaye angalau unamjua kwa undani. Katika dunia ya leo iliyojaa
kila aina ya chanagamoto sababu nyepesi hazifai kuwa sababu za wewe kuachana na
mpenzi wako.
Kuwa mwalimu kwa mwenzako kwa yale mambo
ambayo unaona anakukosea badala ya kutaka kuachana naye. Kuachana na mtu
mnayependana nae leo ni kupanda mbegu ya mauvivu baadaye.
Angalia vizuri sababu zako za kuachana kama ni ngumu huenda kusiwe
na la kufanya ila, kama ni hizi hizi za
kuchelewa kurudi bila kujua sababu we unaona hafai. Kama ni hizi za simu yake
kupigwa mara nyingi bila kujua mpigaji we unakasirika na kumuona Malaya! Fikiri
sana. Kupoteza ni rahisi sana kuliko kutafuta. Ahsanteni.
ramadhanimasenga@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni